
Alitaja kundi hilo kuwa linaundwa na matajiri ambao wengi wao ni wakwepa kodi mashuhuri, watoroshaji nyara na maliasili za nchi, watoroshaji madini, wafalme wa magendo na viongozi waliojitajirisha kupitia rushwa na mikataba mibovu.
Kwa mujibu wa Sitta, katika kundi hilo wamo pia mawakala wa maovu mbalimbali nchini ambao kwa ujumla wao wameamua kuwa baada ya uchaguzi mkuu 2015, nchi iongozwe na mtu ambaye pia ni mpenda utajiri kwa njia za mkato.
“Katika mazingira haya inasikitisha kwamba viongozi wengi hususani wenye uroho wa madaraka na mali, wamejiguza kuwa ni wachekeshaji wa mfalme.
“Wengine ni wabunge, mawaziri. Watu hao wanaonekana kumuunga mkono na mara nyingine kujipendekeza na kumsifia kiongozi wanayejua maovu yake kwa mategemeo ya hatimaye kupewa fedha ama vyeo,” alisema Sitta.
Sitta aliongeza kuwa watu hao walianza kujipambanua miaka miwili iliyopita kwa harambee mbalimbali kwa baadhi ya makanisa, misikiti na makundi mengine kwa kuchangia fedha.
“Harambee zimekuwa zikitangazwa kwa mbwembwe na kelele katika baadhi ya makanisa na misikiti na makundi mengine ya kijamii kwa kuchangia fedha ambazo kwa hesabu nilizonazo kwa kipindi cha miaka miwili ni kiasi cha sh bilioni saba,” alisema Sitta.
Alisema kuwa kwa mkakati huo, ukusanyaji wa kodi na mapato mengine ya serikali utadorora kwa sababu matajiri waovu wanamuunga mkono mtu ambaye akishika madaraka atawaachia mianya ili wasilipe kodi.
“Mtu hawezi kuchangia milioni 60 kwa sababu anampenda yule anayechangisha harambee. Anatoa fedha hizo kama kitangulizo ili na yeye aje asamehewe milioni 200,” alisema.
Alisema mbali na matokeo hayo, pia huduma zote za jamii na kipato cha kila Mtanzania kitapungua na hatimaye misingi ya umoja na usawa itabomoka na kulitumbukiza taifa katika machafuko.
CHANZO; TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment