CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimemuomba Rais Jakaya
Kikwete kuvunja Baraza la Mawaziri kisha awaondoe wanaotajwa kuwa
mizigo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, wakati wa uzinduzi wa Rasimu ya Sera
ya Chadema ya Mabadiliko ya Tabianchi, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi,
John Mnyika, alisema Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni itakwenda kuwabana
mawaziri hao katika mkutano wa Bunge utakaoanza kesho.
Alisema
mawaziri hao ambao ni wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wamekuwa
wakitajwa na wabunge wenzao katika mikutano ya ndani na katika mikutano
ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Katibu wa Itikadi na
Uenezi, Nape Nnauye, lakini hawachukuliwi hatua.
“Kama wabunge wa
CCM, Kinana na Nape hawakuwa wanafiki, basi wabunge wao wawe wa kwanza
kuchukua hatua kabla mawaziri vivuli hatujawashughulikia.
“CCM
wamekuwa wakiwazungumzia mawaziri mizigo na Rais Kikwete hajawahi
kuwashughulikia, wanajaribu kuwakwepesha kwamba watakwenda kujadiliwa na
Kamati Kuu yao, kama Kinana hakuwaelekeza wabunge wake sisi tutaifanya
kazi hiyo.
“Sisi tunawaambia Kinana na Nape, wasome Katiba ya
nchi, Bunge ndilo lenye uwezo wa kuwawajibisha wabunge, sasa Bunge
liwawajibishe au rais aliyewateua avunje Baraza la Mawaziri.
“Kati
ya wanaolalamikiwa amekuwa akisemwa Waziri wa Mifugo, lakini wanaogopa
kumsema Waziri wa Kilimo, sasa waziri wetu kivuli atakwenda kumbana,”
alisema Mnyika.
Akizungumzia rasimu yao, alisema majanga mengi ya
asili yakiwamo ukame, njaa na mafuriko chanzo chake ni mabadiliko ya
tabianchi.
Alisema Serikali haijaweza kushughulikia matatizo ya
mabadiliko ya tabianchi, kutokana na sheria ya mazingira ya mwaka 2004
kupitwa na wakati.
“Asilimia 70 ya majanga ya asili chanzo chake
ni mabadiliko ya tabianchi, kama hatutachukua hatua mapema uhai wa Mlima
Kilimanjaro utakuwa shakani kutokana na kupungua kwa theluji.
“Lakini pia chanzo cha mgao wa umeme tunaambiwa ni kupungua kwa kina cha maji, hii pia chanzo chake ni mabadiliko ya tabianchi.
“Kupitia
rasimu hii, tunaomba mawazo na maoni ya wananchi na kisha tutafanya
utekelezaji wa kuibana Serikali juu ya sera hii,” alisema Mnyika.
Katika
hatua nyingine, Makamu wa Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) na
Katibu Mkuu wa kwanza wa Chama cha Wafanyakazi Madaktari na Wafamasia
(TMDPWU), Dk. Rodrick Kabangila, amejiuzulu nyadhifa hizo baada ya
kuchaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Kanda ya Ziwa Magharibi.
Alisema amechukua uamuzi huo kuondoa mgongano wa kimaslahi kati ya vyama anavyoviongoza, madaktari na Chadema.
“Pamoja
na mambo mazuri niliyohusika katika kuongoza madaktari na kuwa na moyo
wa kuendelea kufanya hivyo, bado kuna mambo mengi hayaendi vizuri ambayo
ni ya kimfumo katika Serikali ya CCM ambayo yanaendelea kudidimiza
huduma za afya.
“Mifano mizuri katika hili ni urasimu usio na
maana katika usambazaji wa dawa na vifaa tiba, kutojali wataalamu,
ufisadi na uzembe kuanzia wizarani, taasisi zake kama bohari ya dawa
hadi katika vituo vya afya,” alisema Dk. Kabangila.
No comments:
Post a Comment